KWA MTINI JIFUNZENI - EMAGK SITE

Latest

This website was designed to help college student especially those who takes engineering course for review, past paper and other learning material. And teacher for review.

Wednesday, April 26, 2023

KWA MTINI JIFUNZENI

 

KWA MTINI JIFUNZENI. (MAJIRA YA KIANGAZI)

MAJIRA NA NYAKATI:

SEHEMU YA 1.

Kila jambo lina majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.  Mhubiri 3:1


Nyakati zimekusudiwa kutujengea umakini, ustadi na hekima ya wakati. Nyakati zinatufanya tujue na tuelewe kuwa hatupaswi kutembea kwa mazoea bali kwa busara na hekima tukitambua kuwa tunapaswa kubadilika na kubadili tunayofanya kutokana na nyakati na wakati tuliona.

 

 

Ni vyema uelewe uko kwenye wakati gani? na ni vitu gani? vya kufanya au kuacha kwenye wakati huo ili uendelee kustawi Zaidi. Huuitaji kuiga maisha ya mtu, unahuitaji kujua majira uliopo na mambo ya msingi unayopaswa kufanya ndani ya majira hayo.

Ndugu yangu wakati wa kiangazi miti hupukutisha majani ilikupunguza kiwango cha maji kinachochukuliwa na jua maana jua huwa kali sana. Lakini pia ni wakati ambao miti huongeza urefu wa mizizi yake ilikutafuta maji ili kukabiliana na uhaba wa maji. Je uko kipindi cha kiangazi? Kipindi ambacho unahitajika kupunguza baadhi ya matumizi. Na kuongeza juhudi katika utafutaji. Kipindi ambacho hata muonekano wako wa kuvutiaa uliokuwanao wakati wa masika umepotea, watu wakikuangalia wanashindwa kujua umekufa au huko hai? Kama miti mingi wakati wa kiangazi ilivyo. Maana baadhi ya miti huonekana kama imekufa lakini kumbe iko hai. Ndugu yangu inawezekana uko wakati huu kwenye biashara yako au huduma yako. Watu wakiangalia biashara au huduma yako wanashindwa kuelewa imekufa au bado ipo? Wengine unaweza kuwasikia wakisema ni afadhali afunge tu imeshakufa hii, ameshashindwa huyu, kwa umri huu hawezi kuolewa tena. Ndugu yangu kwa mtini jifunzeni, Huu ni wakati wa kupunguza baadhi ya vitu, ni wakati wa kuongeza urefu wa mizizi yako kutafuta maji ili kuhakikisha unabaki salama au biashara, huduma yako inabaki salama. Punguza maneno hakuna haja ya kuwajibu, kuwa bize kwenye kukuza mizizi yako. Ikifika wakati wako wa masika waishaingilie ndoa yako, biashara au huduma yako,uwe stori ya kufurahisha na kufundisha katikati ya jamii. Watu waje kuchukua notes kwako namna na njisi ulivyostahimili na kukua wakati wa kiangazi huku wengine wakiishia kuuwa biashara, ndoa, huduma kwa papara na maamuzi mabovu juu ya wakati huo.  Ila kumbuka mti wowote unaozembea kurefusha mizizi yake kutafuta maji wakati wa kiangazi hufa kwa kukosa maji. Ndivyo ilivyo kwetu sisi pia hatupaswi kuzembea maana twaweza kufa kwa uzembe au kuua biashara na huduma zetu kwa uzembee.

Inawezekana unapitia wakati wa kudharauliwa, watu wakikuangalia wanashindwa kukuelewa na kumuelewa MUNGU wako, wengine watakuambia kwanamna hii kama ni huyo MUNGU bora kuachana naye, wengine wakiangalia hali yako, wanakudhihaki na kukukejeli kwa msimamo wako ulionao kwa MUNGU, Nyakati kama hizi za kukimbiwa na kutokueleweka na watu wako wa karibu hata YESU mwenyewe alizipitia. (huu ni wakati wako wa kiangazi, wakati ambao unapaswa kuzamisha mizizi yako chini Zaidi, uzidi kuzama Zaidi kwenye maombi na Neno. Ukizembea unaweza kufa, kama vile mti wowote unaozembea na kujionea huruma wakati wa kuangazi hufa kwa kukosa maji, ila ile ambayo hujitoa na kutenda kwa akili hustahimili na kuvuka salama.  Zaburi 40:1-5

hakikisha ukiwa kwenye wakati huu wa kiangazi usiruhusu kuongozwa na hisia zako, hata akili zako usizitegemee, (mithali 3:5-8). Bali MUNGU awe tegemeo lako, usije ukajikuta unatumia nguvu nyingi kuzamisha mizizi na nguvu zinakuishia kabla ya kupata maji uliyoyahitaji kuvuka kwenye hali uliyonayo. Kwani ukimtegemea MUNGU atakusaidia na kukuongoza ili kujua ni wapi pa kupenyesha mizizi yako ili kuweza kustahimili na kuvuka kwenye nyakati hizo.

Bado unaweza, mti hupambana hadi siku ya mwisho, iko mingine hukauka kabisa matawi yake na kubakiza shina tu, pindi inapofanikiwa kupata maji huchipua tena. Hivyo hupaswi kukata tamaa unapaswa kupambana Zaidi.

Unaruhusiwa kukausha baadhi ya matawi, lakini kumbuka unatakiwa kuhakikisha unachipusha matawi mengi na mazuri kuliko yale ya mwanzo wakati wa masika yako na kurudisha utukufu wako. Kama miti irudishavyo uzuri na ubora wake wakati wa masika.

Kwa mtini Jifunzeni.

Pia hakikisha haujisahau wakati wa masika yako ambapo kila kitu kinakuelekea wewe, watu wanakukubali, biashara zinaenda, ndugu na jamaa wanakufurahia, unatengeneza pesa ndefu, umepandishwa cheo, kila mtu kazini kwako anakusifia na kukuheshimu. Hakikisha unatumia muda huu kurefusha mizizi yako na kuzalisha mizizi mipya pia na sio kujali muonekno wako pekee yake, ili ukija wakati wa kiangazi ukukute umejiandaa, wakati huo usikutese wala kukuumiza ukukute umejiandaa vyema na muonekano wako unabaki kuwa kama ulivyokuwa kwenye masika yako. Waliotegemea kukuumiza washangae kukuona ukitabasamu, waliotegemea kukuangamiza washangae kukuona ukizidi kunawiri Zaidi. Wewe ni wa maana sana tumia wakati huo kujiimarisha na kuimarisha mizizi yako Zaidi kuliko kujionyesha na kuonyesha urembo na uzuri wako huku ukisahau kudumu kwa maua, majani mazuri na uzuri wa mti hutegemea sana mizizi na upatikanaji wa maji.

HAKIKISHA KILA CHANGAMOTO NA NYAKATI UNAZOKUTANA NAZO ZINAKUIMARISHA BILA KUJALI ZIMETOKA WAPI, KWA LENGO GANI NA ZIMEKUJA NYAKATI GANI.” 

 

 

Usijaribu kulazimisha mambo kabla hazifika nyakati zake, mara nyingi sana watu wanaojaribu kulazimisha mambo kabla ya wakati wake huishia kujiumiza na kuumiza wengine. Daudi alijua hili hakuwa na haraka ya ufalme ingawaje ilikuwa kawaida kwa wafalme wengine kumuua aliekwenye kiti ili wao waupate huo ufalme.

Nafasi ambayo MUNGU amekuahidi unapaswa kusubiri kwa wakati usilazimishe mambo usije kuishia kuumiza na kujiumiza mwenyewe, huku wasiwasi ukikutawala kwenye maisha yako.



PREPARED BY: Minister EMANUEL ISRAEL KANGALA, email: emanuelkangala@gmail.com WEBSITE: EMAGK SITE-INSPIRATION, URL: emaisra.blogspot.com, PHONE NO: 0742859313. Released on 19/04/2023

 

No comments:

Post a Comment